Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuboresha miundombinu pamoja na kuongeza Wataalamu wa Afya ya macho ili kusogeza huduma za uchunguzi na Tiba kwa wananchi.
Hayo yamesemwa leo Machi 7, 2022 na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe kwenye maadhimisho ya wiki ya kuongeza uelewa kuhusu Ugonjwa wa shinikizo la Macho katika hospital ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
Dkt. Sichalwe amesema ugonjwa wa shinikizo la macho hauna kinga ila unaweza kuzuilika na kutosababisha ulemavu wa kutokuona unaoletwa na shinikizo la macho kwa kufanya uchunguzi mapema ili kutambulika na kuanza kutumia Tiba,” amesema Dkt. Sichalwe.
“Matibabu ya ugonjwa wa shinikizo la macho yanapatikana hapa nchini katika vituo vyote vya kutolea huduma ya tiba na kuna wataalamu wa macho ambao wanachunguza na kutoa ushauri,” amesema Dkt. Sichalwe.
Aidha, Dkt. Sichalwe amesema kupitia mwongozo wa tiba na orodha ya dawa muhimu uliozinduliwa mwaka 2021, Serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha hali ya upatikanaji wa dawa za macho inazidi kuimarika.
Vile vile, Dkt. Sichalwe ametoa wito kwa Wataalamu wa afya kuwa zoezi la utoaji wa elimu ya afya ya macho na upimaji unaoendelea kwenye hospitali mbalimbali nchini liwe endelevu.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Madaktari bingwa wa macho Dkt. Christopher Mwanansao ametoa wito kwa jamii kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya kwa kuwa ni mkombozi katika kupambana na ugonjwa huu wa shinikizo la macho pamoja na Magonjwa mengine.
“Bima ya afya imekuwa na mchango mkubwa na kimbilio kwa wagonjwa wa shinikizo la Macho, imekuwa ikilipia dawa, baadhi ya vipimo pamoja na upasuaji,” amesema Dkt. Mwanansao.
Shughuli kuu katika maadhimisho ya wiki kwa Tanzania ni utoaji wa elimu ya Afya ya macho kwa wananchi na upimaji wa presha ya macho kupitia vituo vya tiba vilivyopo kote nchini.
Maadhimisho ya wiki ya ugonjwa wa shinikizo la Macho duniani hufanyika kila wiki ya pili ya mwezi Machi kila mwaka.