Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Prof. Anna Tibaijuka ameishauri Serikali kuja na njia mbadala juu ya tiba ya Covid – 19 huku akipendekeza kuanza kutumika kwa tiba mbadala na njia asilia kwa madai kuwa kama yanayotokea nchi nyingine yangetokea Tanzania bado hatuna uwezo mkubwa wa kukabiliana nayo.
Amesema hakuna jamii yeyote itakayokaa na kusubiria kifo hivyo ni vyema kujihami kwa kuja na mkakati mwingine wa kukabiliana na virusi vya Corona.
”Nasema jamii inahitaji survival strategies, na survival strategies ni kusema sisi wenyewe tiba zetu mbadala zipo wapi, za asilia hakuna jamii yeyote itakayokaa na kusubiri kifo, lazima itaangalia na kujihami, ni lazima tuangalie makabila yetu mbalimbvali yana mbinu mbalimbali za kukabiliana na homa za mapafu, covid 19 wanasema ni mpya lakini si mara ya kwanza kwa homa kama hii kutokea” Amebainisha Prof. Tibaijuka
Na kuongeza kuwa ”Wizara ya Afya na Mh. Andungulile nimeshamwandikia barua rasmi, kusema kwamba ni lazima tuangalie option B, sisemi kwamba tusifanye option A, ikitokea watu wengi wameambukizwa ni lazima tuangalie namna ya kuokoa watu wengi”
Amebainisha kuwa makabila mbalimbali yana mbinu mbalimbali za kukabiliana na homa ya mapafu hivyo anaishauri Serikali kutoa kibali ili watalaamu wa tiba mbadala waje na mbinu hizo kudhibiti Corona.
Aidha amemshukuru Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutanguliza sala mbele, kwani ni kweli kwamba Mungu ametuhurumia hadi sasa bado hatujapata majanga makubwa.
”Naungana na kumpongeza ras wetu, tunaanza na sala, sababu lazima tukili kwamba mungu wetu ametuhurumia, Tumshukuru Mungu wetu, ametuhurumia sababu yale yanayotokea yangefika hapa, hatuna uwezo wa kurespond” Ameongeza Tibaijuka.
Hali kadhalika ameongeza kuwa nchi kama Ghana tayari imeshachukua hatua na watu 33 wamepona kwa kutumia njia mbadala ya mwarobaini na kufukizia wagonjwa na wamepona.
”Na mimi naamini kwamba wataokoka nimeangalia figure leo ghana sasa wameshapona watu 33, wakati holland hakuna aliyepona kwasababu wao wamerudi kwenye muarobaini wanafukizia watu na wagonjwa wanapona” amesisitiza Tibaijuka.