TID amekosoa mwenendo wa muziki wa kizazi kipya kwa baadhi ya wasanii, akieleza kuwa maudhui ya nyimbo nyingi hivi sasa yanabomoa jamii badala ya kujenga kizazi bora.
Akifunguka hivi karibuni kupitia The Playlist ya Times FM, TID amesema kuwa wasanii wengi wameacha kuimba nyimbo zenye jumbe za mapenzi na badala yake wanaimba matusi au kuyaanika wanayoyafanya faragha.
“Jamii haitaki hivi vitu, kwa maana kwamba tunatakiwa tuandike muziki ambao tukikiachia kizazi chetu utazisimamia tamaduni zetu miaka hii na ijayo. Hatutakiwi kuwa na muziki mara watu wameanza kuvua chupi, utamfundisha nini mtoto wangu?” TID alifunguka.
“Unaposikiliza muziki unasikia watu mara sijui kuna ‘kufungua mtaro’, it’s non sense (ni upuuzi). Tunawaelimisha nini… muziki ni maisha, kila mtu anasikiliza… [mwimbaji] anaportray (anaonesha) ni yeye sasa ndiye anayefanya hivi vitu. Ni vitu vya hatari, watoto shuleni wanakuwa mashangingi mapema, msichana anacheza [hovyo] hata akiwa shuleni,” aliongeza.
Alisema Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) linapaswa kuendelea kuwafungia wale ambao wanatoa nyimbo zisizofaa, huku akiwasihi wasanii wenzake kuiga mfano wake wa kutoimba matusi na bado akafanikiwa kuliteka soko la muziki na kushinda tuzo nyingi kwa nyimbo za mapenzi.
“Nawaomba sana wasanii… mimi nimeimba muziki nimebeba mpaka matuzo hadi huko nje na sijaimba matusi yoyote na ndio sababu niko hapa hadi leo, muziki wangu unapendwa napata matamasha naenda kuimba. Decent music is what we need (muziki wa heshima ndio tunaouhitaji),” alisema.
Katika hatua nyingine, mkali huyo wa ‘Girlfriend’ amejipanga kuingia tena kwenye soko la filamu ambapo ameeleza kuwa atashirikiana na Bodi ya Filamu nchini kuhakikisha mradi wake mpya uitwao ‘Girlfriends’ unakuwa na mashiko ya kimaadili na kutangaza uzuri wa Tanzania huku ikiwa na ujumbe wa mapenzi wenye mvuto.
Amesema kuwa tayari ameshazungumza na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kuhusu mpango huo na ameuopokea kwa mikono miwili akimpa ushauri pia.