Siku nne baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumuachia huru aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Habari Tanzania (TBC), Tido Mhando, upande wa Jamhuri umekata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.
Tido alikuwa akikabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya pamoja na shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh. 887.1 Milioni kupitia mikataba miwili aliyoisaini na makampuni ya Startimes na Channel 2 Group Cooperation, akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC kwa lengo la kuingia ubia na makampuni hayo katika kuhama kutoka mfumo wa analojia kwenda mfumo wa dijitali.
Alidaiwa kufanya makosa hayo Oktoba, 2017 akiwa Dubai, Falme za Kiarabu.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alieleza kuwa baada ya kusikiliza pande zote mbili, wamebaini kuwa mshtakiwa hana hatia kwani baadhi ya mikataba aliyoisaini haikuwa na nguvu kisheria kutokana na kutosainiwa na wahusika wengine ambao ni Mwanasheria wa TBC kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2011.
Katika utetezi wake, Tido alisema kuwa alisaini mkataba na Channel 2 peke yake kwakuwa yalikuwa makubaliano ya awali na sio mkataba kamili wa mradi.
Alieleza kuwa mkataba kamili ulikuwa kati ya TBC na Startimes ambao aliusaini yeye pamoja na Mwanasheria wa Shirika hilo.
Upande wa Jamhuri umeeleza kuwa umekata rufaa kwa kesi hiyohiyo kwani msingi wa madai yao ni kwamba mshtakiwa alikiuka sheria ya manunuzi katika kusaini mikataba hiyo.
Jamhuri wameongeza kuwa kutokana na mikataba hiyo, Kampuni ya Channel 2 ilifungua kesi Mahakamani iliyoisababishia Serikali hasara ya Sh. 887.1 Milioni.