Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson ameahidi kuendeleza mshikamano wa Marekani na nchi za Afrika, ili kufuta kauli ya utata iliyotolewa na Rais Donald Trump ikilikashifu bara Afrika.
Ameyasema hayo mara baada ya kukutana na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki ambapo amesema kuwa Marekani itazidi kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika, msimamo ambao uko tofauti na kauli rais Trump ambaye alitumia maneno machafu kuelezea nchi ya Haiti na baadhi ya nchi za Afrika.
“Nafikiri ahadi ya mafungamano ya Marekani na nchi za Afrika iko wazi juu ya umuhimu tunaotoa katika ushirikiano huu, hata Rais ameandika barua yake binafsi kwenda AU,”amesema Tillerson
Aidha, amesema kuwa kuhamasisha amani na usalama, maendeleo na biashara, na utawala bora ni nguzo tatu zinazotumiwa na Marekani katika kushirikiana na Afrika.
Hata hivyo, kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Moussa Faki amesema kuwa ziara ya waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Marekani ni ushahidi tosha kuwa mahusiano kati ya Afrika na Marekani bado ni imara.