Mshambuliaji anaeshikilia rekodi ya kupachika mabao kwenye timu ya taifa ya Australia Tim Cahill, ametangaza kustaafu kuitumikia timu hiyo, ambayo ilishiriki fainali za kombe la dunia nchini Urusi.
Cahil ametangaza maamuzi hayo, huku akiweka rekodi nyingine ya kucheza fainali nne za kombe la dunia mfululizo.
Kwa mara ya mwisho mshambuliaji huyo mwenye umri wa 38, aliitumikia Australia katika mchezo wa mwisho hatua ya makundi dhidi ya Peru ambao walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.
“Leo ni siku maalum kuwafahamisha kuwa, ninatangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa, nimejifunza mambo mengi na kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa wachezaji niliocheza nao kwa nyakati tofauti, ” ameandika Cahill kwenye ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa Twitter.
“Sisemi mengi zaidi ya kumshukuru kila mmoja aliyeniwezesha kufikia malengo ya kulitumikia taifa langu kwa moyo wote.”
“Shukurani zangu za dhati zimuendee kila mmoja, na ninawatakia kila la kheri wachezaji wanaoendelea kulitetea taifa letu la Australia katika mapambano ya soka duniani,” aliongeza.
Cahil ameifungia timu ya taifa ya Australia mabao 50 katika michezo 107 aliyocheza tangu mwaka 2004 alipoitwa kwa mara ya kwanza.