Aliyekua mlinda mlango wa klabu za Manchester United na Everton Tim Howard, ametangaza kustaafu soka, baada ya kucheza mchezo wake wa mwisho akiwa na Colorado Rapids ya Marekani.
Howard, 40, mwezi Januari alisema mwishoni mwa msimu wa ligi ya Marekani (MLS) atastaafu kucheza soka, na kweli ametimiza ahadi yake akiwa na Colorado Rapid.
Mlinda mlango huyo kutoka nchini Marekani ametundika daluga huku akiweka historia ya kucheza michezo 339 ya ligi kuu ya England akiwa na Man Utd, kutwaa ubingwa wa kombe la FA mara moja, na ubingwa wa kombe la ligi (kwa sasa linajulikana kama Carrabao Cup) mara tatu.
Akiwa na timu ya taifa ya Marekani, Howard alicheza mchezo 121, na ameshiriki fainali mbili za kombe la dunia (2010 na 2014). Alitangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya Marekani mwaka 2017.
Alisajiliwa na Everton kwa mkopo mwaka 2006 akitokea Man Utd, na mwaka mmoja baadae alisajiliwa moja kwa moja na klabu hiyo ya Goodison Park. Aliitumikia klabu hiyo katika michezo 413 ya michuano yote kwa kipindi cha miaka kumi.
Kwa sasa Howard anashilikia rekodi ya kuwa mlinda mlango alieokoa michomo mingi katika fainali za kombe la dunia – alifanya hivyo katika mchezo dhidi ya Ubelgiji kwa kuokoa michomo 15 mwaka 2014.
Hata hivyo upande wa klabu, Howard hakustaafu kwa furaha, kufuatia klabu yake Colorado Rapids kupoteza dhidi ya LA FC kwa kufungwa mabao matatu kwa moja.