Waziri wa utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa ameipa jina timu ya mpira wa miguu ya wasichana chini ya umri wa miaka 17 na sasa timu hiyo inaitwa Serengeti girls.
Waziri Mchengerwa ametoa jina hilo leo March 11, 2022 baada ya kuitembelea kambini Zanzibar ambapo inaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo wa marudiano na timu ya Botswana kwa ajili ya kufuzu Kombe la Dunia baadae mwaka huu nchini India.
Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo, benchi la ufundi pamoja na viongozi wa TFF na ZFF Waziri Mchengerwa amesema ameipa timu hiyo jina la Serengeti baada ya kujiridhisha kuwa wachezaji wake wana nidhamu ya kutosha, umahiri na moyo wa kujituma sifa zinazowafanya wakidhi vigezo vya kuitangaza mbuga ya Serengeti duniani kote.
“ Kuanzia sasa timu hii itaitwa Serengeti Girls, Pelekeni sifa za Serengeti duniani kote, nyinyi ndiyo tunda na moyo wa Tanzania kwa sasa, mkiamua mtuumize roho zetu ni juu yenu, sisi tuna matarajio mengi na nyinyi, na sisi tuna imani kubwa na ninyi na hasa mheshimiwa Rais SamiaSuluhu ana imani kubwa na nyinyi” Amesema Waziri Mchengerwa
Waziri Mchengerwa amewahimiza wachezaji hao wa timu ya Serengeti Girls kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono katika mchezo wao wa tarehe 20 mwezi huu wa Machi dhidi ya timu ya Botswana katika kuhakikisha wanalinda rekodi yao na kulinda heshima ya nchi.
Katika hatua nyingine Waziri Mchengerwa amepongeza hatua ya ushirikiano uliopo kati ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF na Shirikisho la Zanzibar ZFF Katika kuwanoa vijana hao walioweka kambi visiwani Zanzibar tangu tarehe Februari 23, akisema hatua hiyo ni ushirikiano wa hali ya juu katika kukuza vipaji vya vijana hao.