Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya
Jamii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Buyungu, wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma
Mhe. Aloyce Kamamba amesema timu zote za taifa zifanye maandalizi ya kutosha ili
kuwakilisha vema taifa katika mashindano ya kimataifa.
Mhe. Kamamba amesema hayo Septemba 2, 2022 baada ya kupokea na kujadili taarifa
iliyowasilishwa na Wizara hiyo kwenye kamati hiyo kuhusu utendaji wa taasisi za
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA)
pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
“Sisi kama kamati tumesisitiza Wizara kwamba timu zote za taifa ziwe za wanawake,
wanaume ama walemavu zipate muda wa kutosha kwa ajili ya maandalizi, isiwe muda
mfupi. Ipate muda wa maandalizi wa kutosha pamoja na fedha ili kile cha muhimu
katika timu hiyo kama imeandaliwa vizuri kiweze kupatikan.a kwa timu kufanya vizuri
kwenye mashindano mbalimbali” amesema Mhe. Kamamba.
Timu hizo za taifa zinasimamiwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo
ni muhimu kwa taifa katika kusimamia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini.
Naye Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul kwa niaba ya
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema siri
kubwa ya mafanikio ya Wizara hiyo ni ushirikiano mkubwa kati ya Viongozi wa Wizara
na watumishi wote kuhakikisha malengo ya kuwatumikia watanzania katika sekta za
Utamaduni, Sanaa na Michezo yanafikiwa.
Ili kuhakikisha vipaji vya Sanaa na Michezo kwa vijana vinaendelezwa, Naibu Waziri
Mhe. Gekul amesema wanafunzi wanaofanya vizuri katika mashindano ya
UMITASHUMTA na UMISSETA wataendelezwa kuptia shule maalum za michezo 56
ambazo ni mahususi kwa kuendeleza vipaji vya Sanaa na Michezo.
Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Saidi Yakubu amesema
kuwa Wizara imetenga bilioni 2 kuhakikisha shule 56 za kulea vipaji vya wanamichezo
zinakuwa na miundombinu ya michezo ambayo itasaidia kukuza na kuendeleza vipaji
michezo mbalimbali nchini na kuongeza kuwa Wizara hiyo imetenga kiasi cha Bilioni 10
kuhakikisha kunakuwa na viwanja saba vyenye ubora unaotakiwa kimataifa kwa
michezo mbalimbali.