Jeshi la polisi jimbo la Enugu nchini Nigeria linawashikilia watu 9 kwa tuhuma za kuwabaka waumini wa kike wanaoenda kwenye ibada za mikesha.

Msemaji wa jeshi la polisi katika jimbo hilo, Ebere Amaraizu amesema kuwa ukamataji wa watuhumiwa hao umefanikiwa kutokana na taarifa za kiintelijensia.

Alisema kuwa watu hao walikamatwa katika kanisa lililopo eneo la Akpasha, Magharibi mwa jimbo hilo. Jina la kanisa na waathirika lilihifadhiwa kwa sababu za kimaadili na ueledi. Alisema watu hao walikamatwa Jumamosi majira ya saa nane usiku baada ya kuwekewa mtego.

Amaraizu alisema kuwa vitendo hivyo vya ubakaji vilikuwa vikifanywa kwa waumini wa kike walipotoka nje kwa lengo la kwenda kujisadia, wakati ibada ikiendelea ndani.

“Vitendo hivi visivyokubalika vimekuwa vikifanywa wakati ibada ikiendelea, kwa waumini wa kike waliotoka nje. Wabakaji walikimbia baada ya kufanya uhalifu huo,” Vanguard inamkariri Amaraizu.

Alisema watuhumiwa wako mikononi mwa polisi wakisaidia upelelezi na kwamba utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Bob Junior atoa siri ya kushindwa kufanya vizuri kimuziki
Video: Rekodi ya Lissu yatikisa kimataifa, Jaji Mkuu abana majaji