Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko – CPB, Kanda ya Ziwa imewaondoa hofu wakazi wa ukanda huo na viunga vyake, kuwa imejipanga kukabiliana na baa la njaa kwa kuongeza uzalishaji kutoka tani 5500 hadi tani 20,000 kwa msimu wa 2023/2024.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Mwanza, Kaimu Meneja wa CPB Kanda ya Ziwa, Alfred Kalimenze alisema zao la mkakati kwa ukanda huo ni Mpunga, hivyo wananunua mpunga kwa wakulima, na kuchakata katika mashine zao na kuwauzia wananchi wa kawaida na kusambaza katika nchi jirani.
Amesema, ‘’Baada ya kuchakata huo Mpunga tunapaki katika ujazo toifauti tofauti ili mradi kila mmoja aweze kununua bidhaa yetu kulingana na uwezo wake, lakini pia tunauza katika nchi za jirani zinazotuzunguka kama vile Rwanda, Uganda, na Sudani Kusini.’’
Kalimenze ameongeza kuwa, ili kuhakikisha wananchi wa kanda ya ziwa wanapata huduma bora, wanawauzia mchele grade one Sh. 2700 kwa kilo, wakati huko sokoni mchele kama huo wanauziwa 3200 hadi 3000 na kwamba CPB Kanda ya Ziwa ina mchele wa kutosha tani 100 ambao wanatarajia kuuza kwa Wananchi kwa bei nafuu.
Aidha ameongeza kuwa, katika kukabiliana na baa la njaa ukanda wa Ziwa CPB pia inatarajia kununua mazao mengine kama Maharage tani 1000 na Choroko ili wananchi waweze kupata chakula mchanganyiko chenye ubora na kwa bei nafuu na kwamba bidhaa hizo zinapatikana katika vituo vya mauzo vilivyopo katika Mikoa ya Kagera (Rusumo), Shinyanga na Mwanza.
‘’Mkulima, anapotuletea mazao yake tunamlipa kwa wakati pesa zao, na CPB Kanda ya Ziwa inawauzia bidhaa iliyo bora na kwa bei nafuu kwani imefungua vituo vya ununuzi wa Mpunga katika vituo vitatu ambavyo ni Buchosa, Mpanda na Mpanda Lyonga,” amesema Kalimenze.
Naye Afisa Masoko na Mauzo wa CPB Kanda ya Ziwa, Ally Mango alisema kuwa kiwando chao kina uwezo wa kuchakata tani 96 za mpunga kwa siku lakini kutokana na kukosekana na malighafi kwa wingi, wamefanikiwa kuzalisha tani 594 tu tangu kiwanda hicho kianzishwe mwaka jana.
”Baada ya kuchakata tani 5594 za Mpunga tulifanikiwa kupata tani 3994 za Mchele ambapo tani 1400 ziliuzwa nje ya nchi na tani zilizobaki tumeuza ndani ya nchi hivyo tulipata Sh. Billioni 7.1”, alisema Mango.
Amesema, katika msimu wa mwaka 2023/2024 watachakata tani 20,000 za mpunga ambapo wakiuza mchele wanatarajia kupata Sh. Billioni 26 na kwamba changamoto waliyonayo ni uzalishaji mdogo ukilinganisha na mahitaji ya soko hivyo wanajipanga kutoa elimu kwa wakulima na kuwataka waongeze kilimo cha zao hilo kwa tija.