Mbunge wa Mtama, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amekumbushia tukio la kutishiwa bastola lililotokea jijini Dar es Salaam, miaka miwili iliyopita.
Amezungumzia tukio hilo bungeni, wakati Bunge lilipokuwa limekaa kama kamati kujadili bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya mwaka wa fedha wa 2019/2020.
Nape aliwasilisha hoja hiyo wakati wabunge walipokuwa wakijadili hoja ya Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), aliyekuwa ameondoa shilingi kwenye mshahara wa waziri baada ya kutoridhishwa na majibu ya Serikali kuhusu wananchi wanaouawa, wanaopotea, wanaopigwa risasi na wanaoteswa katika mazingira ya kutatanisha.
“Mwenyekiti, hili tukio la mimi kutishiwa kwa bastola limekuwa likisemwa sana, lakini ni muda mrefu nimekuwa kimya kwa miaka miwili sasa, Mwenyekiti, kwa kweli kufanya siasa katika maisha ya watu si busara kabisa, nakumbuka siku natishiwa, alikuwepo OCD wa wilaya, alikuwapo RPC, lakini kwa bahati mbaya tangu tukio hilo litokee, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya aliyehusika ingawa anajulikana,”amesema Nape
Awali, Msigwa alipokuwa akiwasilisha hoja yake, aliitaka Serikali itoe taarifa za watu waliowahi kupigwa risasi, kuteswa na waliowahi kutekwa katika mazingira ya kutatanisha.
Kwa mujibu wa Msigwa, kitendo cha Serikali kukaa kimya juu ya matukio hayo, kinatia shaka jinsi inavyoshughulikia matukio hayo na kwamba ukimya huo unachochea mwendelezo wa matukio hayo.
Hata hivyo, Mbunge wa Serengeti kupitia CCM, Chacha Ryoba, aliwashangaa wabunge wa Chadema kwa kile alichosema kwamba pamoja na kutaka Serikali ieleze hatua ilizochukua juu ya matukio mbalimbali ya uhalifu, wao walimficha dereva wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), wakati ndiye shahidi muhimu katika tukio la mbunge huyo kupigwa risasi mjini Dodoma.
-
LIVE: Rais Magufuli akiwa kwenye Ibaada ya kusimikwa Askofu Mteule Gervas Nyaisonga Jimbo Kuu Mbeya
-
Tatizo watu wa Mbeya hawajazoea kuambiwa ukweli- RC Chalamila
-
Chama cha watu wenye ulemavu wa Ngozi Tanzania chatoa tamko
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema kuwa matukio yote ya uhalifu nchini yamekuwa yakifunguliwa majalada kwa ajili ya kuyafanyia kazi kabla hatua nyingine hazijachukuliwa.