Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema tatizo la ugonjwa wa figo nchini linaongezeka
Akizungumza na Gazeti la Habari Leo Mratibu wa magonjwa ya figo wa Wizara na Dkt. Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Linda Ezekiel, amesema kuwa takwimu zinaonesha Tanzania ina watu 600,000 wenye ugonjwa wa figo.
Aidha Dkt. Linda Alisema chanzo kikubwa cha magonjwa ya figo ni kisukari, shinikizo la juu la damu, homa ya ini, maambukizi ya Ukimwi na maambukizi ya magonjwa mengine ya bakteria hususani UTI.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Linda amesema takwimu zinaonesha asilimia 0.1 ya watu barani Afrika wana magonjwa ya figo.
Amesema takwimu za hospitali hazitoi picha halisi kwa kuwa wagonjwa wengi wanaokwenda hospitali wanakuwa katika hatua ya kupata huduma ya kusafishwa figo.
“Mwakani Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na WHO, watafanya utafiti mkubwa nyumba kwa nyumba kwa maeneo yatakayochaguliwa ili kuangalia kuna mfumo gani wa maisha ikiwemo uvutaji wa sigara, aina ya vinywaji anavyotumia, aina ya mazoezi anayofanya, shughuli anayofanya na lishe ili kubaini mambo yanayomweka mtu katika hatari ya kupata magonjwa ya figo,”amesema.
Muhumbili yafunga mashine kusafishia figo Amana
Dkt. Linda ameeleza kuwa vipimo vya magonjwa ya figo vinapatikana kwenye hospitali zote za Mikoa, Kanda na Taifa huku gharama ya matibabu ya figo ni kubwa kwa kuwa kupandikiza figo nchini ni Sh milioni 30 na endapo mgonjwa ataenda nje ya nchi gharama zinakuwa mara tatu zaidi.