Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil, Adenor Leonardo Bacchi ‘Tite’ ametangazwa kuinoa timu ya Flamengo inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo mpaka mwishoni mwa mwaka 2024.

Klabu hiyo yenye maskani yake katika jiji la Rio de Janeiro ilitangaza kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kuwa benchi la ufundi la Tite litaundwa na wasaidizi sita waliofanya naye kazi pamoja kwa miaka sita kwenye timu ya taifa ya Brazil.

Tite mwenye umri wa miaka 62, amekua bila ya kazi tangu Brazil itolewe hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Dunia na Croatia Desemba mwaka jana, atasimama kwenye benchi la ufundi la timu hiyo kwenye mchezo dhidi ya Cruzeiro Oktoba 19.

Flamengo ilimtimua kocha Jorge Sampaoli Septemba mwaka huu baada ya raia huyo wa Argentina kushindwa kunyakua taji na timu hiyo.

Sampaoli alimbadili kocha Vitor Pereira kutoka Ureno aliyetumia miezi mitatu kuinoa timu hiyo.

Flamengo iliondolewa na timu ya Olimpia kutoka Paraguay kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya Copa Libertadores, walipoteza mchezo wa fainali Kombe la Brazil dhidi ya Sao Paulo na inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo ikiwa na pointi 44 katika mechi 26 ilizocheza nyuma ya Botafogo.

Tite aliiongoza Corinthians kushinda taji la Copa Libertadores na Kombe la Dunia la klabu mwaka 2012 kwa kuifunga Chelsea.

Mwakalebela awapa somo Viongozi, Kocha Young Africans
Rage aipongeza Tabora Utd, azionya Simba, Young Africans