Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa mwenendo wa hali ya hewa kwa mikoa ya kaskazini inayopakana na nchi ya Kenya, ikieleza kuwa kiwango hafifu cha upepo hakiwezi kahamisha nzige kutoka katika nchi hiyo na kuingia Tanzania.
Meneja wa kituo kikuu cha utabiri wa hali ya hewa cha TMA, Samweli Mbuya, amesema upepo unaovuma sasa ni wa kasi ya kilomita 20 hadi 25 kwa saa na ili nzige wahame unatakiwa kufika kilomita 28 kwa saa.
Upepo ukitulia nzige huweka makao kwa hiyo kwa sasa kuna kiwango kidogo cha upepo kuja Tanzania na hii ni hali inayotarajiwa kwa siku kumi zijazo yaani kuanzia Februari 11 hadi 21, 2020.
“Hawa wadudu ili waruke lazima kuwe na mazingira ya kuruka kwa hiyo taarifa hii inalenga kujiandaa” amesema Mbuya.
Amewataka wataalamu wa sekta husika kufuatilia taarifa ya hali ya hewa ili kuweza kukabiliana na nzige.
Naye mkurugenzi wa TMA Agness Kijazi amesema utabiri haumaanishi kuwa nzige wapo nchini Tanzania na kwamaba upepo unaweza ukahama usiwe na muelekeo wa kuja nchini.