Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) imesema kimbunga Jobo kimepungua nguvu kwa haraka baada ya kuingia katika mazingira yenye mzunguko wa upepo kinzani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo imesema kwa sasa kimbunga hicho ni hafifu.
Hata hivyo Kimbunga hafifu ‘Jobo’ kinatarajiwa kusababisha vipindi vya mvua kubwa katika maeneo machache hususani ya ukanda wa Pwani kadri kinavyosogea nchi kavu kwa siku ya leo na kesho Aprili 25, 2021. Pia mamlaka hiyo imetoa tahadhari kuwa uwepo wa kimbunga hicho hafifu utasababisha mawimbi makubwa baharini.
Maeneo yanayotarajiwa kupata athari ya moja kwa moja ni pamoja na mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na Kisiwa cha Unguja.
Wananchi wanashauriwa kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.