Mamlaka ya hali ya hewa nchini (TMA), imetoa utabiri wa hali ya hewa kwa mwezi Oktoba, Novemba na Disemba ukionyesha maeneo mengi ya nchi yatapata mvua chache na hivyo kusababisha athari ikiwemo upungufu wa chakula.
Mkurugenzi mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi amesema hayo leo Septemba 9, jijini Dar es salaam na kuwashauri wakulima kupanda mbegu za mazao zisizo hitaji maji mengi.
“Mvua zitanyesha kwa kiwango cha chini cha wastani hadi wastani katika maeneo mengi na zikitarajiwa kuambatana na vipindi virefu vya ukavu kuanzia wiki ya pili ya Septemba, 2020” amesema Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi amesema kuwa vipindi hivyo ni kwa mikoa wa Kagera, Mwanza, Geita, Mara, Simiyu, Shinyanga na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma katika wiki ya tatu ya Septemba 2020, zikitarajiwa kuishia Januari, 2021.
Aidha, ameeleza kuwa athari hizo zitajitokeza si kwa Tanzania pekee bali pia ni kwa nchi za Afrika Mashariki huku akieleza athari hizo kwa sekta mbali mbali hapa nchini ikiwemo wafugaji na wakulima.