Nyota wa Ligi Kuu ya England, Sandro Tonali na Nicolo Zaniolo wamehojiwa na mamlaka za lItalia kwa madai ya kucheza kamari kinyume cha sheria.
Wawili hao waliondoka kwenye kambi ya mazoezi ya timu ya taifa ya Italia, Alhamisi usiku, baada ya kuzungumza na polisi na inasemekana walisindikizwa na kipa wa zamani, Gianluigi Buffon kwa ajili ya mahojiano.
Taarifa rasmi kutoka Shirikisho la Soka Italia (FIGC) ilisema: “Shirikisho linaeleza kuwa alasiri ya leo ofisi ya mwendesha mashtaka wa Turin ilitoa taarifa za nyaraka za uchunguzi kwa wachezaji Sandro Tonali na Nicolo Zaniolo, ambao kwa sasa wanafanya mazoezi na timu ya taifa katika kituo cha ufundi cha Shirikisho cha Coverciano.”
“Bila kujali aina ya vitendo hivyo, kwa kuamini kuwa katika hali hii wachezaji hao wawili hawapo katika hali ya lazima ya kukabiliana na majukumu yaliyopangwa siku chache zijazo, shirikisho limeamua kuwaruhusu kurejea kwenye klabu zao kwa ulinzi mkali.”
Tonali anatarajiwa kurejea Newcastle United, huku Zaniolo akirejea Aston Villa ambako alijiunga akitokea Galatasaray kwa mkopo.
Mastaa hao wanaweza kukumbwa na adhabu ya kufungiwa endapo itabainika walijihusishwa na michezo ya kamari ambayo inakiuka sheria za soka nchini Italia.
Inadaiwa Zaniolo alibeti kamari kwa kuihusisha AS Roma ambayo awali alikuwa akiichezea chini ya kocha Jose Mourinho.
Pia kwa mujibu wa ripoti kiungo wa Juventus, Nicolas Fagioli anachunguzwa na polisi lakini hakujumuishwa katika kikosi cha Italia kwa ajili ya mechi za kufuzu Fainali za Euro.