Imefahamika kuwa Kocha Mkuu wa Chelsea, Mauricio Pochettino anapiga hesabu za kuwasajili Washambuliaji Ivan Toney na Victor Osimhen kwenye kikosi chake ili kuokoa jahazi wakati dirisha la Januari 2024, litakapofunguliwa.
Chelsea kwa sasa inashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England ikiwa imeshinda mechi moja tu kati ya sita za kwanza.
Mmiliki wa Chelsea, bilionea Todd Boehly alifanya usajili wa wachezaji tisa kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu, lakini kwenye usajili huo mpya hakuna ambao umeweza kufanya vizuri hadi sasa.
Kwa sasa inaelezwa kuwa Pochettino bado anahitaji wachezaji zaidi waletwe kwenye kikosi chake na hilo amewaambia mabosi wake.
Ripoti zinadai kwamba Washambuliaji Toney na Osimhen wapo kwenye orodha ya wanaosakwa na kocha huyo kutoka nchini Argentina.
Pochettino mwenye umri wa miaka 51, anaamini kwa kuwaongeza washambuliaji hao wataweza kuipa Chelsea nguvu kubwa kwenye safu yao ya ushambuliaji.
Hata hivyo kwenye saini ya Toney Chelsea huenda ikaingia katika vita kali na mahasimu wao wa London, Arsenal kutokana na wao wanamuhitaji Mshambuliaji huyo anayethaminishwa na Brentford kuwa na thamani ya Pauni 80 milioni.
Lakini, kuhusu Osimhen, Chelsea watalazimika kuvunja benki kwa sababu SSC Napoli hawatakuwa tayari kumuuza Mshambuliaji wao huyo kwa bei ya kutupa.
Chelsea itashuka uwanjani baadae leo Jumatatu (Oktoba 02) kukipiga na majirani zao wa London, Fulham katika mchezo wa Ligi Kuu ya England.