Klabu ya Manchester City imelenga kumsajili mwamba wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na ipo tayari kumlipa Pauni 13 milioni kwa mwaka ili tu asaini kukipiga Etihad.
Timu hiyo inayonolewa na Kocha Pep Guardiola ilibeba taji lake la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, wakati ilipoweka rekodi ya kunyakua mataji matatu makubwa ndani ya msimu mmoja.
Na kwenye dirisha lililopita, Guardiola aliboresha kikosi chake kwa kuwasajili Josko Gvardiol, Matheus Nunes, Jeremy Doku na Mateo Kovacic.
Lakini, sasa anahusishwa na mpango wa kumchukua mchezaji mwenye uzoefu zaidi na dili hilo litafanyika mwishoni mwa msimu huu.
Kinachoripotiwa ni kwamba kiungo veteran wa Real Madrid, Toni Kroos ndiye ambaye kwa sasa amewekwa kwenye rada za Man City.
Na kwamba Mjerumani huyo akitua tu Etihad basi mshahara wake atalipwa karibu mara mbili ya kile kiwango anachopokea huko Bernabeu.
Kroos mwenye umri wa miaka 33, alijiunga na Madrid akitokea Bayern Munich mwaka 2014 na mahali hapo amebeba karibu kila taji aliloshindania.
Amenyakua Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tano, likiwamo moja alilobeba Bayern, La Liga mara tatu na Klabu Bingwa Dunia mara nne. Mkataba wake wa sasa utafika tamati Juni 2024.
Huko Bernabeu, Kroos kwa sasa analipwa Pauni 6.8 milioni kwa mwaka, lakini Man City itamlipa Pauni 13 milioni na itampa dili la miaka miwili, hivyo ana uhakika wa kupiga mkwanja mrefu Pauni 26 milioni.