Kiungo mkabaji Mukoko Tonombe na winga Tuisila Kisinda waliosajiliwa Young Africans wakitokea AS Vita ya DR Congo, wanatarajiwa kutua nchini leo majira ya saa 7:20 mchana, sanjari na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said.

Hersi alifunga safari hadi mjini Kinshasa DR Congo, kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya usajili ya wachezaji hao wawili, na juzi usiku alithibitisha kukamilisha taratibu zote za usajili wa Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda.

Meneja wa Klabu ya Young Africans, Hafidh Saleh amethibitisha wachezaji hao wawili watawasili leo mchana na viongozi wa klabu hiyo pamoja na wanachama na mashabiki watakaojitokeza Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

“Suala la maandalizi ya mapokezi na hamasa ya kuwapokea jambo hilo lipo mikononi mwa akina Antonio Nugaz, ila taarifa tuliyonayo wanawasili kesho mchana,” amesema Hafidh.

Kuhusu Kocha Mkuu, Hafidh amesema: “Hili jambo la kocha lipo kwa viongozi, wa juu ndio wanaweza wakalizungumzia zaidi, kwa sasa bado makocha waliopo ndio wanasimamia mazoezi na yanaendelea vizuri.”

Kikosi cha Young Africans kinaendelea na mazoezi katika Uwanja wa Chuo cha Sheria jijini Dar es Salaam chini ya makocha wasaidizi, Riedoh Berdien na Said Maulid.

JPM: Nimepitia majina yote ya watiania
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Agosti 20, 2020