Meneja wa klabu ya West Brom Tony Pulis amefichua siri ya mazungumzo yake na meneja wa Arsenal Arsene Wenger, waliyoyafanya mara baada ya mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England mwishoni mwa juma lililopita.
Pulis amedai kuambiwa na meneja huyo kuhusu mustakabali wake, baada ya kumuuliza kama ataendelea kubaki klabuni hapo, kufuatia shinikizo linaloendelea dhidi ya baadhi ya mashabiki ambao wanampinga kwa kuutaka uongozi wa Arsenal usimpe mkataba mpya.
Pulis aliwaambia waandishi wa habari kuwa, mzee huyo kutoka nchini Ufaransa alimwambia bila kificho kwamba, ataendelea kubaki klabuni hapo na ana uhakika wa kusaini mkataba mpya wakati wowote kabla ya msimu huu kufikia kikomo.
Wawili hao walifanya mazungumzo ya faragha, huku mashabiki wa Arsenal wakigubikwa na hasira za kupoteza mchezo wa ligi kwa kufungwa mabao matatu kwa moja siku ya jumamosi.
Kufuatia kipigo hicho Arsenal imeporomoka hadi katika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi ya England, na hatua hiyo imekuja kufuatia ushindi wa Manchester United wa mabao matatu kwa moja walioupata jana dhidi ya Middlesbrough.