Kikosi cha Toto Africans leo jioni kitafahamu hatma ya kuendelea kuwa sehemu ya timu za ligi kuu kwa msimu ujao wa 2017/18 au la, kwa kumenyana na mabingwa watetezi Young Africans kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.

Toto Africans ambao kwa sasa wapo kwenye msitari wa kushuka daraja wanahitaji kupata ushindi ili kufufua matumaini ya kupigania nafasi ya kusalia ligi kuu kwa msimu ujao.

Katika kuhakikisha suala hilo linafanikiwa katika mchezo wa leo, uongozi wa klabu hiyo ya jijini Mwanza umewandaa kisaikolojia wachezaji wao, kwa kuwataka wapambane hadi tone la mwisho la jasho lao.

Afisa habari wa Toto Africans Cuthbert Japhet, amezungumza na Dar24 na kueleza mipango walionayo kabla kikosi chao hakijashuka dimbani jioni ya leo kupepetana na Young Africans.

Japhet amesema wanatambua umuhimu wa mchezo wa leo na wana kila sababu ya kupambana, kwa sababu kama watashindwa kufanya kile kinachokusudiwa watakuwa wamejichimbia kaburi.

“Watu wengi wanaamini uswahiba wetu na Young Africans unaweza kuharibu mazingira ya mchezo wa leo kwa kuwaachia ili waendelee kujisafishia njia ya ubingwa, lakini ninakwambia ndugu yangu leo patachimbika.”

“Hatutaki kushuka daraja wakati nafasi ya kupambana bado tunayo, tuna kila sababu ya kujitetea ndani ya dakika tisini, tunaamini uwezo wa kikosi chetu ni mkubwa sana, na kila mmoja ameshaambiwa namna ya kufanya ili kutimiza jukumu la kuondoka na point tatu leo.” Amesema Japhet.

Mchezo huo pia una faida kubwa kwa Young Africans, endapo watashinda watakua wamejiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa Tanzania bara kwa mara ya tatu mfululizo.

Young Africans wanaongoza msimamo wa ligi wakiwa na point 65 huku wakisaliwa na michezo miwili, na watani zao wa jadi Simba SC wanaoshika nafasi ya pili wana point 65 na mchezo mmoja mkononi.

Toto Africans wapo katika nafasi ya 15 kwa kufikisha point 29 na kama watashinda leo watakuwa na point 32 ambazo zitaendelea kuwaweka kwenye matumaini ya kubaki ligi kuu.

Mbarak Yusuf Afutiwa Kadi Nyekundu, Yamgharimu Mwamuzi
Brad Pitt afunguka kuhusu fikra za kujitoa roho baada ya kutoswa na Angelina Jolie