Mshambuliaji Wilfried Zaha huenda akakaidi mipango ya viongozi wa klabu ya Crystal Palace ya kufanya mazungumzo ya kusaini mkataba mpya, baada ya kiwango chake kuendelea kukua siku hadi siku.
Mwenyekiti wa Crystal Palace Steve Parish jana alizungumza na shirika la utangazaji la Uingereza BBC na kueleza dhamira ya kuzungumza na mshambuliaji huyo, ambaye aliamua kurejea kwenye nchi yake ya asili ya Ivory Coast mwishoni mwa mwaka jana, baada ya kupata wakati mgumu wa kujumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England cha wakubwa.
Crystal Palace wamejipanga kumlipa Zaha mshahara wa Pauni 100,000 kwa juma, huku wakiamini ofa hiyo itakua kichoheo kikubwa kufanikisha lengo la kumbakisha mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24.
Mapema hii leo taarifa zilizochapishwa kwenye gazeti la The Sun la nchini England zimeeleza kuwa, Zaha huenda akakataa kufanya mazungumzo na uongozi wake kwa lengo la kushinikiza kuuzwa mwishoni mwa msimu huu.
Klabu ya Tottenham Hotspurs inaongoza kutajwa katika harakati za kumsajili Zaha, na tayari imeelezwa kiwango cha pesa kilichotengwa kwa ajili ya uhamisho wake ni Pauni milioni 15.
Meneja wa Spurs Mauricio Pochettino anaongoza vita ya kutaka kumsajili mshambuliaji huyo, na tayari ameutaka uongozi wa juu wa klabu hiyo kuhakikisha wanafanikisha harakati za kumuhamishia Zaha kaskazini mwa jijini London.
Mwishoni mwa juma lililopita Zaha alifunga moja ya mabao mawili ya Crystal Palace dhidi ya Chelsea, hatua ambayo iliendelea kudhihiridha kukua kwa kiwango chake cha kusakata kabumbu.