Kufuatia agizo la Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuweka gharama za usajili wa huduma za habari zinazotolewa kwa njia ya mtandaoni wanaharakati mbalimbali wamehoji mkakati huo wa kudhibiti maudhui mtandao.
Kwani wanaharakati, watumiaji wa mtandao na wamiliki wa mitandao hiyo wameona serikali imeamua kutumia mwanya huo kubana uhuru wa kujieleza.
Mmoja ya wanaharakati anayefahamika kwa jina la Jonathan amehoji juu ya tozo zilizowekwa kwani amedai kuwa sio bloggers wote wanatumia mitandao hiyo kufanya biashara, Amesema.
-
TCRA yatoa siku 14 za usajili wa huduma mtandaoni
-
TCRA yashauri jinsi ya kusuluhisha changamoto kesi za mitandaoni
“Suala tata ni kuhusiana na tozo zilizowekwa maana sio bloggers wote wanafanya biashara sana kuna wengine wanatoa elimu tu ya afya au michezo na hakuna faida yeyote wanayopata hivyo itakuwa ngumu kwa wao kuendelea kuchapisha kwenye mtandao, tunataka kutoa ushirikiano wa dhati lakini kiuhalisia ni ngumu hivyo inabidi TCRA watoe elimu kwanza,”Jonathan aeleza.
Aidha, Mwenyekiti wa wamiliki wa blogu, Johakimu Mushi amesema Tanzania bloggers hawana tatizo kabisa na suala la kujisajili maana wanajua umuhimu wa kusajiliwa ni kuonekana kwamba wanatambuliwa na kazi wanazozifanya na itasaidia kuangalia maadili.
Serikali nayo imesema imefanya hivyo kudhibiti baadhi ya taarifa zinazotoka nje ya nchi na zinazosambaa ndani ya nchi zinazoichafua nchi, maana kumekuwa na upotoshaji mkubwa kupitia habari za mitandaoni.