Mamlaka ya Mapato nchini – TRA, imetangaza ongezeko la kodi ya majengo itakayotozwa na kupitia ununuzi wa umeme kuanzia Julai, 2023 kufuatia mabadiliko ya Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo, Sura 289.
Taarifa ya TRA imeeleza kuwa, nyumba ya kawaida iliyokuwa inatozwa Shilingi 12,000 kwa mwaka, sasa itatozwa Shilingi 18,000 sawa na Shilingi 1,500 kwa mwezi kiwango kitakachotekelezwa kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2023 ambayo pia yanapanua wigo wa ukusanyaji wa kodi hiyo, kwa kujumuisha nyumba zilizopo maeneo yote ya wilaya.
Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa, Nyumba za ghorofa katika maeneo ya majiji, manispaa za halmashauri za miji zilizokuwa zikitozwa Shilingi 60,000 kwa kila sakafu kwa mwaka, sasa zitatozwa Shilingi 90,000 kwa kila sakafu, sawa na Shilingi 7,500 kwa mwezi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, “utekelezaji wa kutoza kodi hii ya majengo kwa kufuata mabadiliko tajwa hapo juu, umeanza Julai, 2023. Viwango hivyo vya utozaji kodi ya majengo vilivyobadilika na vitaendelea kutozwa kupitia ununuzi wa umeme.”
Mapema hivi karibuni, Serikali ilipendekeza kufanyika marekebisho hayo kupitia hotuba ya bajeti iliyosomwa bungeni Juni, mwaka huu ambapo liliombwa kufanya marekebisho ya kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo, Sura 289 kwa kuongeza maeneo yote ya wilaya, isipokuwa majengo yaliyosamehewa.