Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini, William Lukuvi amesimamisha ujenzi wa uwanja wa mpira wa watu watano watano katika fukwe ya Coco (Coco beach), jijini Dares Salaam uliokuwa ukiendelea katika eneo hilo na kuvunja uzio uliowekwa.
Akiwa ziarani kwenye fukwe hizo Waziri Lukuvi amewapa onyo viongozi wa Kinondoni (Meya na Mkuu wa Wilaya) kutokuwa na tamaa na sehemu za wazi ambazo ni mali za umma.
Amesema kuwa hakuna Halmashauri yenye mamlaka ya kubadili matumizi ya ‘Opening Space’ mpaka ofisi za makimishina wa mikoa zijue lakini sio kubadili.
Aidha Waziri amewataka makamishna wasaidizi wote kupekua sehemu zote za wazi zinazotamaniwa na kuzirudisha na kusema kuwa zibaki kwa matumizi ya umma.
Pamoja na hayo Lukuvi amepiga marufuku wananchi kutozwa fedha wanapoingia kwenye fukwe mbalimbali nchini, fukwe ni eneo la wazi kwa kila mtu hivyo mmiliki wa eneo akipewa kibali cha kujenga ufukweni anatakiwa kutambua kwamba wananchi lazima waingie
Amebainisha kuwa ufukwe ni mali ya Watanzania na ni huru kwa kila mmoja na kuagiza Coco kuendelea kufanyiwa usafi na kutunzwa na wananchi waendelee na shughuli zao.