Rais wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Moise Katumbi amesema klabu yake imefikia makubaliano rasmi ya kushirikiana katika masuala mbalimbali na vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC.
Katumbi amesema hayo baada ya kumaliza kikao na mabosi wa Simba SC na baadaye kwenda kushuhudia mchezo wa Ufunguzi wa Wekundu wa Msimbazi dhidi ya mabingwa wa Afrika, AI Ahly kutoka Misri.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Katumbi amesema anaamini ushirikiano wa klabu hizo mbili utasaidia kuzipa mafanikio na hatimaye kufanya vyema katika mashindano mbalimbali ya kimataifa wanayoshiriki.
Katumbi amesema amefurahi kuona Simba SC imepata nafasi ya kushiriki mashindano ya African Football League kwa sababu kupitia michuano hiyo, klabu pamoja na wachezaji watapata nafasi ya kujitangaza kwa timu nyingine za Ulaya.
“Ninawapongeza sana viongozi wa Simba SC kwa hatua ambayo wamefika, kuongoza klabu ya soka si jambo dogo, kupata mafanikio katika mashindano ya CAF kunatokana na juhudi na jitihada viongozi na wachezaji.
Mazembe kushirikiana na Simba SC haijaanza sasa, tulianza huko nyuma tulipomchukua Mbwana Ali (Samatta), tukampata pia UIimwengu (Thomas), tunaishukuru pia Serikali ya Tanzania kwa kutupokea,” amesema Katumbi.
Kuhusu nafasi ya Simba SC katika michuano ya African Football League, Katumbi amesema mafanikio ya klabu ndio yamewafikisha katika ngazi hiyo na heshima waliyopata ya kucheza mechi ya ufunguzi ni ishara soka la Tanzania limepanda.
“Haya mashindano yataleta mambo mazuri, yataleta fedha nyingi katika timu zetu, Simba SC, Mamelodi na TP Mazembe kwa upande wa SADC, itafungua fursa mbalimbali, niseme tu Simba SC imestahili kufika hapa ilipo,” amesema Katumbi.
Mmiliki huyo wa mabingwa hao wa zamani wa Afrika amewataka mashabiki wote wa soka nchini kuwashangilia Simba SC katika michuano hiyo, kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili dhidi ya Al Ahly.
“Jana, nilikuwa upande wa Simba, hakuna Mazembe, hakuna Young Africans, mimi pia nitaiombea Simba ifanye vizuri katika mechi yao,” Katumbi ameongeza.
Bosi huyo amesema pia amefurahi kuona Simba SC imekubali kuwasaidia katika maandalizi ya mechi watakazochezea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuahidi ushirikiano huo utazaa matunda kwa klabu zote mbili.
Kwa sasa Simba SC ina mchezaji mmoja iliyemsajiliwa kwa mkopo akitokea TP Mazembe ambaye ni mshambuliaji, Jean Baleke.
TP Mazembe inatarajia kucheza mechi yake ya michuano ya AFL kesho Jumapili (Oktoba 22) dhidi ya Esperance de Tunis kutoka Tunisia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.