Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania ‘TPBRC’, imetoa miezi miwili kwa mabondia, mapromota na washereheshaji wa mchezo huo kuwa na leseni zitakazowatambulisha.

Makamu wa Rais ‘TPBRC’, Nassoro Chuma, amesema wahusika mchezo huo wanapaswa kuwa na leseni za utambuzi, lengo likiwa kuzuia watu wasiokuwa rasmi kujipenyeza na kuharibu wasifu wa masumbwi.

Chuma amesema leseni za kutambua idadi ya mabondia, mapromota na washereheshaji wa mchezo huo zimeanza kutolewa mwezi huu Julai hadi Septemba Mosi, mwaka huu.

Amesema ‘TPBRC’ haitamtambua mtu yeyote asiyekuwa na leseni na haitamruhusu kufanya kazi hadi atakapokidhi vigezo.

“Tunataka kuendelea kuufanya na mchezo wa masumbwi kuwa heshima, shirikisho halipo tayari kufanya kazi na watu wasiokuwa na sifa ambao wengi wao ni waharibifu,” amesema Chuma.

Ameongeza kuwa leseni kwa wanamasumbwi itatolewa kwa ada ya sh. 10, 000 huku mapromota wakilipa sh. 50, 000 na washereheshaji sh. 20,000.

Bondia Saleh Kassim aliitaka TPBRC kutoa elimu kwa mabondia hasa wa mikoani kuhusu umuhimu wa kuwa na leseni.

“Nimesikia hili la mabondia kuwa na leseni lakini wengi hawaelewi umuhimu wa kuwa na leseni, hivyo wakati taratibu za kupata leseni likiendelea na wao watoe elimu,” amesema Kassim.

Ashley Young kufanyiwa vipimo England
Miguel Gamondi aanika mipango Young Africans