Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini (TPBRC), imeweka wazi mikakati yake katika mchezo huo, ikitangaza kuwa itahakikisha inainua vipaji vya mabondia wanawake.
Katibu Mkuu wa Kamisheni hiyo, George Silas, amesema lengo lao ni kupata idadi kubwa ya mabondia wa kike ili weweze kucheza mapambano makubwa na kuileta nchini mikanda kama ilivyokuwa kwa upande wa wanaume.
“Tutahakikisha kila pambano linalochezwa lazima liwepo la wanawake ili kupata mabondia wengi wanawake ambao watakuwa na uwezo wa kucheza mapambano makubwa na kuwa mabingwa,” amesema Silas.
Ameongeza kuwa kuna mabondia wengi wanawake wana vipaji isipokuwa wanashindwa kufika mbali kutokana na kukosa watu wa kuwaunga mkono.
Mbali na hilo, amesema muda wowote kuanzia sasa watatoa maamuzi rasmi ya tukio lililomfanya bondia Hassan Mwakinyo kugomee pambano lililokuwa lifanyike Septemba 29, mwaka huu, dhidi ya mpinzani wake, Julius Indongo kutoka Namibia.
“Mwakinyo tayari ameleta vielelezo vyake kwa nini alishindwa kupanda ulingoni pamoja na mwandaaji wa Paf Sports Promotion, hivyo muda wowote tutawaeleza Watanzania maamuzi tuliyoyachukua ili wajue kinachoendelea na maagizo tuliyopewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ya kupeleka maelezo, tayari tumeshatekeleza,” amesema Katibu huyo