Watendaji wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ‘TPLB’ imesema msimu ujao 2023/24 wataendelea kuwa wakali kwa klabu zote zitakazovunja sheria na kanuni zilizowekwa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TPLB Almas Kasongo amesema, kila msimu wanajipanga kusimamia kanuni na hawatamuogopa au kumuhurumia mtu/klabu yoyote itakayoenda kinyume na kanuni hizo.
Kasongo amesema msimu ujao hawataangalia miundombinu pekee bali wataingia mpaka ndani ya klabu kuhakikisha zinaajiri watu wenye sifa ambao watasimamia na kufanya shughuli za klabu kwa weledi ili ziweze kutoka hapo zilipo kwenda kwenye mafanikio zaidi.
Kasongo amesema kuwa msimu ulioisha walijikita zaidi katika kufungia miundombinu ambayo ilikuwa haitoi nafasi kwa timu kucheza mpira vizuri kutokana na ubovu hususani sehemu ya kuchezea (Pitch).
“Ni kweli msimu uliopita tumefungia viwanja vingi, lakini msimu ujao tutakuwa wakali zaidi kuliko tulivyokuwa katika msimu uliopita, tumeongeza wigo zaidi wakusimamia, hatutasimamia miundombinu tu, tutaangalia timu za vijana katika klabu, je eneo la utawala lina watu sahihi ambao wanatosha kuwepo katika timu husika”, amesema Kasongo.