Bodi ya Ligi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetuma salamu za pole kwa viongozi wa Polisi Tanzania FC, kufuatia kikosi cha klabu hiyo kupata ajali wakati kikitoka kwenye mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United Mara FC, utakaochezwa Julai 14.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Polisi Tanzania, kupitia akaunti rasmi ya Instagram ya Polisi Tanzania imeeleza namna hii: Timu yetu imepata ajali wakati ikitoka mazoezini leo. Baadhi ya wachezaji wameumia.
Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Hassan Juma amesema kuwa kwa sasa wanashughulikia afya za wachezaji pamoja na wale ambao wameumia na taarifa rasmi zitatolewa.
TPLB wameandika kwenye ukurasa wao wa Instagram: “Bodi ya Ligi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) pokea kwa masikitiko taarifa ya tukio la basi la timu ya Polisi Tanzania FC (likiwa na wachezaji), kupata ajali huko mjini Moshi.”
“Timu hiyo ilikuwa inatoka mazoezini wakijiandaa na michezo iliyosalia ya Ligi Kuu ya Vodacom 2020/2021.”
“Poleni sana Polisi Tanzania na tunawatakia nafuu ya mapema majeruhi wote. Amin!”
Wakati huo huo Uongozi wa klabu ya Azam FC imeungana na TPLB kutoa salamu za pole kwa Uongozi wa Polisi Tanzania.
“Azam FC tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kupata ajali kwa timu ya Polisi Tanzania, wakati wakitoka mazoezini leo Ijumaa asubuhi.”
“Tunaungana na Watanzania wote, kutoa pole kwa uongozi wa @polisitanzaniafootballclub na tunamuomba Mwenyezi Mungu awasimamie na kuwaponya majeruhi wote na kuwarejesha kwenye hali zao za kawaida.” Imeeleza taarifa ya Azam FC iliyowekwa kwenye kurasa za mitanfao ya kijamii za klabu hiyo.