Baada ya kuamalizika kwa Msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/21, Bodi ya Ligi (TPLB) imefunguka na kutoa sababu za kuchelewa kumalizika kwa msimu huo.
Ratiba ya awali ya Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/21 iliyotolewa mwanzoni mwa msimu, ilionesha Ligi hiyo ingefikia tamati mwezi Mei, lakini ilikuwa tofauti.
Afisa mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo amesema kuna mambo kadhaa yalikua kikwazo ambayo yaliwalazimu kubadilisha ratiba ya Ligi Kuu Mara kwa mara.
Amesema jambo kubwa na zito lililochangia kuchelewa kumalizika kwa msimu 2020/21 ni msiba wa aliyekua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli.
Amesema baada ya kufariki kwa kiongozi huyo mapema mwezi Machi, nchi iliingia katika kipindi cha maombolezo kwa siku 21, hali iliyofanya baadhi ya shughuli kusimama ikiwemo michezo ya ndani.
Sababu nyingine iliotajwa na kiongozi huyo wa TPLB ni ushiriki wa Simba SC na Namungo FC kwenye michuano ya vilabu Barani Afrika.
Simba SC ilishiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hadi hatua ya Robo Fainali na Namingo walishiriki Kombe la Shirikisho hadi hatua ya Makundi.
Ligi Kuu Tanzania Bara Msimu 2020/21 ilifikia tamati Julai 18, huku Simba SC wakitetea taji lao kwa mara ya nne mfululizo.
Katika Ligi hiyo klabu za Ihefu FC, Gwambina FC, JKT Tanzania na Mwadui FC zilishuka daraja, huku Mtibwa Sugar na Coastal Union zikinusurika baada ya kushinda michezo ya Play Off dhidi ya Transit Camp na Pamba FC.