Klabu ya Young Africans imepewa onyo na Bodi la Ligi ‘TPLB’ kupitia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, baada ya kukutwa na hatia ya kuvunja Kanuni za Ligi Kuu wakati wa mchezo dhidi ya Azam FC uliopigwa Azam Complex, Chamazi-Dar es salaam April 06.
Taarifa ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya TPLB imeeleza kuwa Young Africans ilifanya kosa la kuingia Uwanjani kupitia Mlango usio Rasmi katika mchezo huo.
Kwa kuzingatia Kanuni ya 17 ( 21&60) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za mchezo, Young Africans imetozwa faini ya Shilingi Milioni Mbili na kupewa onyo kali.
Pia klabu hiyo Kongwe imepigwa faini ya Shilingi Milioni Moja kwa kosa la Mashabiki wake kumrushia chupa Mwamuzi msaidizi wa mchezo dhidi ya Azam FC, adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa Klabu.
Wakati Young Africans ikikumbwa na adhabi hizo, Simba SC nao imetozwa faini ya Shilingi Milioni Moja kwa kosa la Mashabiki wake kurusha chupa uwanjani wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Caostal Union iliyokubali kulala mabao 2-1, Uwanja wa CCM Mkwakwani April 09.
Mashabiki wa Simba SC walifanya kitendo hicho baada ya Mshambuliaji Meddie Kagere kufunga bao la ushindi dakika za lala salama kipindi cha pili.
Simba SC imepewa adhabu hiyo kwa kuzingatia kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa Klabu.