Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Diana Masalla amesema kuwa, mwananchi yeyote atakayefichua wakwepa kodi na TRA ikafuatilia na hatimaye kodi hiyo ikagundulika ni kweli ilikuwa imekwepwa na ikakusanywa, mwananchi aliyetoa taarifa hizo za ukwepaji kodi atalipwa asimilia 3 ya kodi iliyokusanywa lakini haitazidi shilingi milioni 20.

Masalla ameyasema hayo wakati wa Jukwaa la Biashara na Uchumi lililofanyika katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu ambalo lengo lake ni kujadili fursa, changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji wilayani humo na kuzitafutia ufumbuzi.

“Natoa wito kwa wananchi na washiriki wa jukwaa hili kuhakikisha mnawafichua wakwepa kodi wote kwa sababu watu hao wanaiibia Serikali yetu mapato na wanarudisha nyumba jitihada za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi wake,” Amesema Masalla.

Aidha, Masalla amewahimiza wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki jukwaa hilo kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa pindi wanapokuwa wamefunga biashara kutokana na sababu mbalimbali ili kuepuka kuendelea kutozwa kodi au kuonekana wamekaidi kulipa kodi.

“Ni muhimu kutoa taarifa TRA pale ambapo mfanyabiashara amefunga biashara yake lakini pale anapofungua ni muhimu pia kuitaarifu TRA ili kuepuka kuendelea kutozwa kodi unapofunga biashara na pia kuanza kutozwa kodi sahihi pale unapofungua biashara,” amesisitiza Masalla.

Naye, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Wilaya ya Busega David Mateko amempongeza Meneja wa TRA Mkoa wa Simuyu kwa kutoa elimu ya kodi kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara mkoani humo pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na hatimaye kuifanya Wilaya ya Busega kuwa wilaya ya pili kati ya wilaya 5 za mkoani Simiyu kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yanayosimamiwa na TRA.

 

Hukumu ya kifo yatolewa, walimuua mwanafunzi kwa moto
Samia mgeni rasmi semina wabunge wanawake Jumuiya ya Madola