Mamlaka ya Mapato tanzania (TRA), imetolea ufafanuzi juu ya tapeli aliyekamatwa akiwa na kitambulisho cha mamlaka hiyo.

Ufafanuzi huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa elimu kwa mlipakodi, Richard Kayombo  alipozungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam, na kusema kuwa mtuhumiwa huyo siyo mfanyakazi wa mamlaka hiyo, ni tapeli na kitambulisho alichokutwa nacho ni feki.

Hayo yamejiri baada ya kusambaa kwa video fupi kwenye mitandao ya kijamii inayomuonesha Hassan Muluguru, mkazi wa Twangoma akiwa chini ya ulinzi na kukiri kuwa amemtapeli mwanamke mmoja.

Kayombo amesema baada ya kufuatilia taarifa hizo wamegundua kuwa mtu huyo alikuwa anakusanya fedha kwa kuchukua taslimu kutoka kwa wafanyabishara njia ambayo mamlaka hiyo haitumii kwani fedha zote hutumwa benki au kwanjia ya simu.

Aidha amesema kwa sasa wameamua kuanza kutumia utaratibu wa ‘Name and shame’ yaani kusambaza picha na majina yao matapeli wanaowakamata ili jamii iweze kuwatambua na kuchukua tahadhari.

“mtu ambaye anabainika anafanya vitendo kama hivi tunatumia mbinu ya kusambaza ili afahamike kwa jamii, pamoja na hayo vyombo vinavyohusika vinafanya uchuguzi ili kubaini nani yupo nyuma yao, ili waweze kuchukuliwa hatua kali ” amesisitiza Kayombo.

Ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pale wanapoona viashiria vya matapeli wanaotumia jina la TRA kuwachukulia pesa kinyume cha taratibu, kwa kufika katika ofisi za TRA au kupiga simu kwa namba za bure 0800750075, 0800780078 au wakampiga picha na kutuma WhatsApp 0744233333.

Na amewatahadharisha kwa wale wanaopigiwa simu kuwa wanatakiwa kulipa kiasi cha fedha ili maduka yao yasikaguliwe ni utapeli hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kufika ofisi za TRA endapo watapata wasiwasi.

 

 

 

Simba SC yakwama kwenye machimbo ya almasi
AfDB kuipa Tanzania zaidi ya Sh 1 trilioni kujenga uwanja wa ndege Dodoma