Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekanusha taarifa zilizokuwa zimeenea mitandaoni kuwa wameanza oparesheni ya kusimamisha magari barabarani na kudai risiti za mafuta kulingana na kiwango cha mafuta kinachoonekana kwenye gari husika.
Taarifa hizo zilizosambaa kwa kasi ndani ya kipindi cha siku mbili kwenye mitandao ya kijamii zilieleza kuwa maafisa wa TRA wamekuwa wakiangalia ‘gauge’ ya gari na kudai risiti kwa mhusika, ikiwa ni sehemu ya oparesheni iliyotokana na ongezeko la shilingi 40 kwa kila lita moja ya mafuta.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo ameiambia Clouds FM kuwa taarifa hizo ni za uongo na kwamba kinachofanyika ni kuhakikisha vituo husika vya mafuta vinatoa risiti kwa wateja wake na wateja kudai risiti wawapo kituoni hapo.
“Hiyo ni taarifa ya uzushi na ya uongo. Ukweli ni kwamba kampeni tunayoendelea nayo ya kukagua risiti kwenye biashara mbalimbali na biashara mojawapo ni za mafuta,” alisema Kayombo.
“Katika kukagua risti kwa upande wa mafuta huwa tunaenda kwenye vituo vya mafuta kuangalia kama mwenye kituo anatoa risti. Lakini vilevile wale waliowekewa mafuta palepale kituoni na sio barabarani, Je, wamepewa risiti kabla ya kuondoka?”Aliongeza.
Alisema kuwa kwa mujibu wa sheria, mtoa huduma ambaye atabainika kutompa risiti mteja wake atakabiliwa na faini ya papo kwa papo ya kati ya shilingi milioni 3 na milioni 4.5.
Alifafanua kuwa kwa mteja wa mafuta ambaye ataondoka bila kudai risiti, akiwa bado yuko kituoni atakumbwa na faini ya kati ya shilingi elfu thelathini hadi shilingi milioni moja na nusu.