Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata bidhaa za magendo, zilizoingizwa nchini kwa njia ya panya, ambazo zimeisababishia Serikali hasara ya kutokulipa kodi ya Sh bilioni 3.3 huku zikiwa na thamani ya jumla ya Sh bilioni 4.

Aidha, imetaja maeneo korofi yanayotumika kuingiza bidhaa hizo kuwa ni Bagamoyo, Saadani, Mlingotini, Mbegani Juu, Mbweni, Ununio, Kunduchi, Kawe na Msasani.Maeneo mengine ni Kigamboni, Ufukwe wa Bamba, Kimbiji, Pemba Mnazi, Kibada, Nyamisati, Kisiju, Mkuranga, Ubungo na katikati ya jiji.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Elimu kwa Mlipakodi, Diana Masala amesema kuwa bidhaa hizo, zimekamatwa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Bidhaa hizo zilikamatwa katika msako uliofanywa na Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Idara ya Upelelezi Tanzania.

Amesema kuwa bidhaa hizo zimekamatwa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba mwaka huu kutokana na utaratibu wa kufanya doria na msako kwa pamoja katika maeneo ya mwambao wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

“Bidhaa zilizokamatwa ni majokofu yaliyotumika, luninga, simu za viganjani, kanga, vitenge, chakula na mafuta ya kupikia. Kufanikiwa kukamatwa bidhaa hizi kumetokana na ushirikiano kati ya TRA, Jeshi la Polisi, JWTZ, matumizi ya vifaa vya kielekroniki na taarifa kutoka kwa wasamaria wema,” alisema Masala.

Hata hivyo amesema kuwa bidhaa za magendo, zinaathiri uchumi wa Taifa kwa ujumla na kwamba wataendelea kudhibiti bidhaa za magendo kwa kufanya doria nchi kavu na bandarini pamoja na misako ya kushtukiza katika maeneo hayo korofi.

 

Majaliwa awaagiza waalimu kuishi karibu na shule wanazofundishia
Stereo alivyofunga mwaka na zigo la penzi zito kwa rapa Chemical