Serikali imesema kuwa mapato yatokanayo na kodi ya majengo yanayokusanywa na Serikali yameongezeka baada ya jukumu hilo kukabidhiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikilinganishwa na ilivyokuwa chini ya Halmashauri.

Hayo yamesemwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Bukoba, Wilfred Lwakatare (CHADEMA), aliyetaka kujua Serikali inazipa Halmashauri ushauri gani wa kitaalam wa hatua za kuchukua ili kuziba pengo la kibajeti.

Dkt. Kijaji amesema kuwa baada ya makusanyo yatokanayo na kodi za majengo kuanza kukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA katika Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji , yalipanda hadi kufikia Sh. bilioni 34.09 mwaka wa fedha  2016/2017 ikilinganishwa na Sh. bilioni 28.28 zilizokuwa zimekusanywa na Serikali za Mitaa mwaka wa fedha 2015/2016.

“Makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.6 ya makusanyo halisi yaliyopatikana kutoka Halmashauri husika kabla ya kodi hiyo kuhamishiwa TRA hali inayodhihirisha kuwa, TRA imefanya kazi nzuri katika kukusanya mapato ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa na Halmashauri hizo 30 katika mwaka wa fedha 2015/16.”amesema Dkt. Kijaji.

Amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kunakuwepo ufanisi katika ukusanyaji na matumizi ya kodi zote zinazokusanywa ndani ya Serikali na kwamba Halmashauri zote zinapata mgao wa fedha kwa kuzingatia makisio ya bajeti zao na makusanyo ya mapato yote ya Serikali.

Hata hivyo, Dkt. Kijaji amesema kuwa Serikali inatambua kuwa kodi ya majengo imekuwa ikichangia kwa sehemu kubwa mapato ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji katika kutekeleza mipango na utoaji wa huduma na maendeleo kwa wananchi.

 

Masha aitosa Chadema, amsifu Rais Magufuli
Serikali yazuia uzinduzi wa ripoti ya HRW