Mamlaka ya Mapato Nchini, TRA imewataka Wafanyabiasha na Watanzania wote kwa ujumla kuwa makini na matapeli wanaotumia jina la mamlaka hiyo kufanya uhalifu wa Mtandaoni.
Wito huo, umetolewa hii leo Agosti 15, 2023 na Meneje wa TRA Mkoa wa Dodoma, Castro John wakati wa uzinduzi wa kampeni ya zoezi lao la Tuwajibike, ambalo linahusiana na uwajibikaji wa utoaji risiti.
Amesema, “tumekuwa tukipata kesi nyingi sana kuhusiana na hao matapeli mitandaoni na hizo changamoto titahakikisha tunazitatua kwa haraka kwa kuendelea kutoa elimu kwa wafanya biashara na Wananchi wote kwa ujumla.”
Hata hivyo, John amesema kwa wale wanaofanya biashara mitandaoni wanatakiwa kuhakikisha wanatoa risiti kwasababu TRA ina wafuatiliaji wa masuala yote ya biashara za Mitandaoni hivyo atakae bainika anaenda kinyume, sheria itafata mkundo wake.
Naye Moja kati ya wafanyabiashara waliotembelewa na TRA, Lupi Mwaikambo ameipongeza Mamlaka hiyo kwa kampeni ya tuwajibike, huku akiitaka iendelee kutoa elimu mara kwa mara kwa jamii.
“TRA elimu hii itolewe kwa wananchi mara kwa mara kwa kuwa ni kitu ambacho kinaonekana hakifahamiki kwenye jamii, elimu ya kudai rist kwa wananchi haipo kwahiyo endapo elimu hii ikatolewa mara kwa mara jamii itafahamu umuhimu wake,” amesema Lupi.