Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kodi Kariakoo umetoa tangazo la kukamata mizigo au bidhaa ambazo hazitakuwa na risiti halali na kuwakumbusha wafanyabiashara wote pamoja na wateja wao kuwa adhabu kali itatolewa kwa wote wasiotoa wala kudai risiti.
Amesema kuwa kwa wasiotoa risiti watatozwa adhabu ya shilingi milioni 3 hadi milioni 4.5 na wale wasiodai risiti watatozwa adhabu ya shilingi milioni 1.5 kwa kila kosa.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Kodi Kariakoo Jijini Dar es salaam, Hashim Ngoda katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari akisema kuwa TRA imeanza kuendesha msako katika maeneo yote kwa wale wasiotoa au kudai risiti wafanyapo manunuzi ya bidhaa mbalimbali.
“Adhabu kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya atakayekaidi tangazo hili ikiwa ni pamoja na ku kamata mizigo au bidhaa zisizokuwa na risiti halali. Kumbuka adhabu kwa wasiotoa risiti ni Sh milioni 3 hadi Sh milioni 4.5 na kwa wasiodai risiti adhabu yake ni shilingi milioni 1.5 kwa kila kosa,”alisema Ngoda na kuwashauri wamachinga wote kudai risiti kila wanapofanya manunuzi yao.
Katika hatua nyingine, Kaimu Meneja huyo aliwajulisha wamiliki wote wa majengo kuwa mwisho wa kulipa kodi ya majengo kwa mwaka 2018/19 ni Juni 30, mwaka huu.
Alieleza utaratibu wa ulipaji wa kodi hizo kuwa nyumba ya kawaida ni Sh 10,000, nyumba ya sakafu ya ghorofa katika majiji, miji na manispaa ni Sh 50,000 pamoja na ghorofa zima katika halmashauri za wilaya ni Sh 20,000.
“Malipo sasa yanaweza kutumika kwa kutumia simu yako ya mkononi hivyo ni vema kulipa kodi mapema ili kuepuka usumbufu usio wa lazima,” alisema.