Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James, amewashukuru wananchi na walipakodi wote kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati wa makusanyo ya mwezi Septemba na Desemba, 2019, amesema ni ishara kwamba, walipakodi kwa ujumla wao, wanaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuongeza mapato ya nchi.

Amewataka watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzingata misingi wa Sheria za kodi ili kuhakikisha kuwa TRA inaendelea kuvunja rekodi ya makusanyo ya mapato kama ilivyokuwa katika mwezi Septemba na Desemba, 2019.

Akizungumza wakati wa mkutano wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi wa nusu mwaka 2019/20 wa mamlaka hiyo James ameleza kuwa, mapato makubwa yanayotegemewa na Serikali ni makusanyo ya kodi.

Aidha ameipongeza TRA kwa kujituma na kuipelekea Serikali kukusanya mapato kiasi cha Sh. trilioni 9.341 sawa na ufanisi wa asilimia 47.67 ya lengo la kukusanya sh. trilioni 19.595 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2019/2020 yaani kuanzia Julai hadi Desemba 2019. 

“Ukiangalia mchanganuo wa makusanyo yote ya Serikali, sehemu kubwa sana ni kodi inayokusanywa na TRA. Kwa msingi huu, TRA inapofanikiwa kukusanya kodi kwa ufanisi mkubwa ndiyo mafanikio ya Serikali katika kutekeleza bajeti inayokuwa imepangwa kwa kipindi hicho,” amesema Katibu Mkuu huyo.

 Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Edwin Mhede, amesema kwamba, mkutano huo wa mapitio na tathmini ya nusu mwaka ulilenga kufanya maboresho katika utendaji kazi ili kuhakikisha kuwa malengo waliyopangiwa na Serikali yanafikiwa.

 Dkt. Mhede aliongeza kuwa, TRA imepewa agizo na Serikali la kukusanya kiasi cha sh. trilioni 19.5 katika mwaka huu wa fedha 2019/20 ambapo pamoja na kufanya vizuri katika miezi ya Septemba na Desemba, 2019, alikiri kuwa bado Mamlaka hiyo haijafikia malengo ya makusanyo kwa asilimia 100.

 Mkutano huo wa tathmini ya utendaji kazi wa nusu mwaka 2019/20 wa TRA ulihudhuriwa na jumla ya washiriki 361 ukihusisha Menejimenti nzima ya Mamlaka, Mameneja wote wa Mikoa na Wilaya kutoka Tanzania Bara na Visiwani pamoja na baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo.

Mfuga nyoka afariki dunia baada ya kung'atwa na nyoka
Mkuu wa majeshi Niger afukuzwa kazi

Comments

comments