Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), imeweka rekodi ya makusanyo ya Shilingi Trilioni 2.088 kwa Mwezi Desemba 2020, kiwango ambacho kinatajwa kuwa hakijawahi kufikiwa katika historia ya ukusanyaji wa kodi nchini.

Taarifa hiyo ya makusanyo imetolewa jana Januari 1, 2020 na Kamishna wa TRA Edwin Mhede katika mkutano wake na waandishi wa habari ambao pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James.

“Tumevunja rekodi yetu wenyewe, hatujawahi kukusanya kiasi hicho katika historia yetu, tunamshukuru Mungu na walipa kodi wote. Hii ni zawadi ya kipekee ya walipa kodi kwa Rais John Magufuli,”amesema Mhede.

Mhede ameyataja makusanyo ya Desemba 2020 kuwa ni Shilingi Trilioni 2.09 sawa na asilimia 101 ya lengo lililowekwa la Shilingi Trilioni 2.07.

Mhede amesema kwa Desemba Idara ya walipa kodi wakubwa imevuka malengo yake kwa kukusanya zaidi ya Sh. Trilioni 1 sawa na asilimia 113 ikifuatiwa na idara ya forodha asilimia 97 na idara ya walipa kodi wa kati na wadogo ambao walifikia aasilimia 85 ya malengo yao.

TRA imekusanya Sh. Trilioni 9.98 katika kipindi cha miezi sita lengo lake la mwaka likiwa ni kukusanya Trilioni 20.3 hivyo kulingana na hesabu za makusanyo ili kufikia lengo la Serikali katika kipindi kilichobaki TRA itapaswa kukusanya kiasi cha Sh. Trilioni 10.32 sawa na wastani wa Sh. Trilioni 1.72 kwa kila mwezi kuanzia Januari hadi Juni.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu James ameupongeza uongozi wa TRA kwa mafanikio hayo huku akitaja suala la risiti za kielektroniki (EFD), kama changamoto ambayo inahitaji kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.

Suala la risiti za EFD linatusumbua sana, hatulifurahii tunalitafutia tiba usiku na mchana. Jambo hapa ni kutotoa risiti, kutoa risiti tofauti na bei halisi na kutotoa risiti, hili litafika mwisho, si suala gumu, tatafanya kila tunaloweza tuondoe hiyo aibu,” amesema James.

Nchi za Afrika zazindua eneo la biashara huria
Tanzia: Mtoto wa Mwalimu Nyerere afariki dunia