Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA, imesema kuwa Serikali ya awamu ya tano ili iweze kuachana na utegemezi kutoka kwa wafadhili, inatakiwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kulipa kodi bila kushurutishwa .
Hayo yamesemwa na Naibu Kamishna wa TRA Charles Kuchele, Mkoani Morogoro wakati wa ziara yake ya kuzungumza na wafanyabiashara nia ikiwa ni kufahamu changamoto zinazowakabiri wafanyabiashara hao.
Amesema kuwa endapo kila mfanyabiashara atalipa kodi kwa hiari yake bila shuruti basi suala la kufikia uchumi wa kati kwa nchi ya Tanzania litawezekana.
“Morogoro ina mchango mkubwa sana kwenye pato la Taifa kwani imekuwa ikifanya vizuri na hii inatufanya TRA tuendelee kuuamini na kuhakikisha changamoto zilizopo zinatatuliwa kwa nguvu zote,”amesema Kuchele.
Hata hivyo amesema kuwa ukusanyaji mapato na kulipa kodi Mkoa wa Morogoro unashika nafasi ya pili jambo alilolipongeza na kuwataka wafanyabiashara kutokata tamaa pamoja na kuwapo kwa changamoto kwenye mashine za kielektroniki EFD’s.