Mamlaka ya Mapato Tanzania, (TRA), imezindua rasmi utoaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta rasmi ikiwa ni pamoja na wamachinga.

Utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara hao unatokana na marekebisho ya sheria ya usimamizi wa kodi ya mwaka 2015 yaliyofanywa na kikao cha Bunge la bajeti la mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo moja ya marekebisho hayo ni kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi.

Zoezi hili linatekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, (TRA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), Wakala wa Usajili, Ufilisi na udhamini (RITA) pamoja na Idara ya Uhamiaji.

TRA kwa kushirikiana na wadau husika hapo juu, ilianza kutekeleza jukumu hilo kwa kuutambua Umoja wa wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuwapatia vitambulisho vya Taifa na Namba ya Utambulisho wa mlipa kodi (TIN) ambapo leo hii baadhi yao wamepatiwa vitambulisho maalum vya wafanyabiashara wadogo kama ishara ya uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho hivyo.

Baada ya mafanikio haya, zoezi la kutambua vikundi mbalimbali vya wafanyabiashara wadogo na kuwapatia kitambulisho cha Taifa na Namba ya Utambulisho wa Mlipa kodi linaendelea kufanyika nchi nzima.

 

Kesi ya Miguna yapamba moto, atupwa Dubai
Lowassa atinga Mahakamani kusikiliza hatma ya viongozi wa Chadema