Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani limetakiwa kuacha tabia ya kujificha kuvizia ajali zitokee katika maeneo hatarishi hasa ya makutano na badala yake wajikite katika kutoa elimu na kusimamia taratibu za uzuiaji wa ajali zinazoweza kuepukika nchini.
Sambamba na hatua hiyo pia Jeshi hilo limetakiwa kufuatilia kwa ukaribu suala la wahanga wa ajali ili kuokoa maisha yao na kuhakikisha wanapata stahiki zao badala ya kufika eneo la tukio kufanya upimaji na kuondoka.
Wito huo umetolea hii leo Novemba 16, 2019 jijini Dodoma na Mbunge wa Iramba mashariki Allan Kiula katika kikao cha kuwakumbuka wahanga wa ajali barabarani kinachofikia kilele chake Novemba 17, 2019 na kuongeza kuwa nidhamu katika utendaji kazi husaidia kuleta mabadiliko.
Amesema kumekuwepo na mtindo wa baadhi ya askari wa barabarani kujificha katika maeneo hatarishi ambayo ajali za mara kwa mara hutokea ili kungoja ajali kitu ambacho si cha kiungwana kinachoenenda kinyume cha maadili ya kazi badala ya kusimamia usalama wa eneo husika.
“Mfano makutano ya barabara ya area C hapa Dodoma pale hutokea ajali nyingi lakini unakuta askari wapo na badala ya kuongoza magari wao hukaa pembeni kitu ambacho si cha kiungwana maana eneo lile linahitaji usaidizi kutokana na ongezeko la watembea kwa miguu, uwepo wa idadi kubwa ya pikipiki na magari,” amebainisha Mbunge Kiula.
Awali akitoa ushuhuda wa ajali Mbunge wa viti maalum Dodoma mjini Fatma Tawfiq amesema ajali nyingi husababishwa na uzembe wa madereva, mwendo kasi, kusinzia na ubovu wa barabara na kwamba endapo sheria zitaangaliwa upya na kuwekewa makali huenda mambo hayo yatapungua na hatimaye kuisha.
“Nikiwa mkuu wa Wilaya nilipata ajali na nilivunjika mguu wangu mara nne sababu ya uzembe wa dereva wa gari lililokuwa likija mbele yetu alitugonga na ilikua ni gari ya serikali na ukiniona natembea naibia ibia usijedhani ni mkogo hapana ni uzembe wa dereva umesababisha leo hii mguu wangu haupo sawa hivyo mamlaka zikemee kwa vitendo mambo kama haya,” amebainisha Bi. Tawfiq.
Naye Mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Rose Tweve amesema wakati umefika kwa vyombo husika kutobagua kwa vyeo au mali katika utoaji wa adhabu kwa wavunja sheria za usalama wa barabarani kwani wengi wa wanaosababisha ajali ni madereva wa serikali ambao mara nyingi huenda kwa mwendo na kuyapita magari mengine bila tahadhari.
“Siku moja dereva wa serikali ametanua bila tahadhari mimi nilikataa kutoka katika upande wangu ulio halali kisheria alishuka akaanza kugomba lakini sikukubali kitendo kile nilimuomba amuite Polisi lakini baadae akaondoka sasa hili lisibague vyombo vya usalama vitenge hat wiki mbili za mfano kuwakamata bila kubagua wote wapate adhabu stahiki itasaidia kurudisha heshima,” amefafanua Bi. Tweve.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Afisa programu wa Tanganyika Law Society (TLS) Mackphason Buberwa amesema utafiti wa Shirika la afya Duniani (WHO), unaonyesha vifo vitokanavyo na ajali za barabarani vinashika namba nane kwani kwa mwaka watu milioni 1 hufa duniani kwa ajali hizo.
Amesema utafiti huo unaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2030 ajali za barabarani zinaweza kushika namba 1 kwa kuuwa watu na kuzitaja sababu zitokanazo na ajali kuwa ni magari yasiyo viwango, barabara mbovu na madereva kutokuwa wastaarabu.
“Na baada ya kuona jambo hili ni tishio ndio maana TLS inapigana toka mwana 2003 juu ya kuona ni namna gani tunaweza kuweka mikakati ya kuzuia mambo kama haya ambayo.huacha alama za makovu ya maisha kwa ndugu zetu wanaopata ajali na familia kukosa msaada wao au kuwaacha yatima,” ameongeza Buberwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha mawakili Dodoma Mary Munisi amesema suala la ufungaji mikanda nalo huchangia ajali kwani sheria inaonesha mtu wa mbele na dereva wafunge mikanda na si abiria wote kitu ambacho kinaleta mkanganyiko hivyo ni vyema zikaangaliwa upya.
Amesema kwa upande wa uvaaji wa kofia ngumu sheria zake zilitengenezwa zamani kipindi ambacho pikipiki ilikua haijawa chombo cha usafiri na kwa sasa inatakiwa kupitiwa upya kwani kanuni zilizopo zimepitwa na wakati na zinahitaji kuboreshwa.
Naye Inspekta wa Polisi kitengo cha usalama barabarani Josephat Mjema amesema sheria zimekuwa hazijaainisha chochote juu ya uendeshaji wa mwendokasi maeneo maalumu kama sokoni, shuleni, hospitali na maeneo maalum na wanapendekeza utumike mwendo kasi wa 30kph badala ya 50kph.
Amesema pia miundombinu isiyofaa na ufinyu wa barabara umekuwa ni tatizo kwani watumiaji ni wengi na mwendo kasi wa magari si rafiki kwani unaweza kusababisha ajali za mara kwa mara hivyo vyanzo vyote vya ajali vinapaswa kuangaliwa upya ili sheria zisimamie mapungufu.
Hata hivyo amesema Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa weledi na kwamba sheria zilizopo zinasimamiwa ipasavyo na kutoa rai kwa viongozi wa serikali kuacha kuwachukulia kama sehemu ya vikwazo kutokana na mara nyingi madereva wao kuto tii sheria za barabarani.