Mshambuliaji wa klabu ya Wolverhampton Wonderers ya England Adama Traoré Diarra, amekataa ofa ya kuitumikia timu ya taifa lake la asili (Mali), na kukubali kujiunga kikosi cha timu ya taifa ya Hispania.

Traore aliitwa kwenye vikosi vya nchi hizo mapema juma lililopita kwa ajili ya michezo ya kimataifa ya kirafiki itakayochezwa mwishoni mwa juma hili, hali ambayo iliibua sintofahamu miongoni mwa wadau wa soka duniani, lakini wengi walihisi angefanya maamuzi ya kuitema Mali, na ndivyo ilivyotokea.

Mali walimuhitaji mshambuliaji huyo mwenye kasi ya ajabu uwanjani kwenda kuchezea kwenye timu yao ya taifa, katika michezo ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Ghana, Oktoba 09 na kisha dhidi ya Iran siku nne baadae.

Hata hivyo kocha wa timu ya taifa ya Hispania, Luis Enrique naye alimjumuisha Traore kwenye kikosi chake cha awali kinachojiandaa na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Ureno na michezo ya michuano ya Nations League dhidi ya Uswisi na Ukraine.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 amelazimika kufanya maamuzi hayo, ambayo yanamuidhinisha kuwa mchezaji halali wa Hispania, baada ya kuzitumikia timu za vijana za taifa hilo chini ya 16, 17, 19 na 21.

Traore alizaliwa mjini L’Hospitalet de Llobregat, Hispania baada ya wazazi wake kuhamishia makazi yao nchini humo wakitokea nyumbani kwao Mali.

FC Barcelona yapata hasara ya mabilioni
Lil Ommy, DJ Sinyorita watajwa Marekani, kuwania Tuzo, Diamond afunika