Shirika la Reli Tanzania – TRC, limeutaarifu umma kuwa Basi la abiria lenye namba T178 DVB mali ya kampuni ya Ally’s Star Bus limepata ajali baada ya kugonga kichwa cha treni chenye namba V951 9006 kilichokuwa kikitokea Stesheni ya Aghondi kuelekea Manyoni katika makutano ya reli na barabara eneo la Manyoni mkoani Singida majira ya alfajiri.
Taarifa iliyotolewa na TRC kupitia Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Jamila Mbarouk imeeleza kuwa ajali hiyo imehusisha basi la abiria lililokuwa likivuka njia ya reli eneo la Kilomita 587 Manyoni na kichwa cha treni na kusababisha majeruhi 25, wanawake saba, wanaume 18 na vifo vya watu 13, wanawake sita, wanaume saba.
TRC imeeleza kuwa itaendelea kuutaarifu umma kadri taarifa zinavyopatikana huku likiwasihi madereva wa vyombo vya moto kufuata Sheria na alama za usalama katika njia ya reli na barabarani zilizowekwa ili kuepusha ajali.
Taarifa hiyo pia imesema Shirika linatoa pole kwa ndugu wa marehemu na Mwenyezi Mungu awape nafuu majeruhi waweze kuendelea na shughuli za kujenga taifa.