Morocco imefanikiwa kuwa nchi yenye treni inayoenda kasi zaidi barani Afrika, inayozinduliwa leo jijini Casablanca.
Treni hiyo ambayo itakuwa ikienda umbali wa Kilemeta 320 kwa saa, itakuwa ikifanya safari zake kati ya miji ya kibiashara kuanzia Casablanca na Tangier.
Kwa kuipa picha ya Tanzania, treni hiyo inaweza kutumia saa 1 na nusu kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma (Km 445).
Mfalme Mohammed VI na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron wamepanda treni hiyo na kusafiri nayo katika safari yake ya kwanza kutoka Tangier hadi Rabat.
Treni hiyo itakuwa na mwendo kasi mara mbili zaidi ya treni ya Afrika Kusini iliyokuwa inaaminika kwa mwendo kasi, ikisafirisha watu kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Johannesburg na wilaya ya Sandton.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari nchini humo, mradi huo umegharimu $2.4 bilioni.