Treni iliyokuwa inaenda kasi jana iligonga watu waliokuwa wakitazama tamasha Kaskazini mwa India na kuua 60 kati yao.
Shuhuda wa tukio hilo ameviambia vyombo vya habari kuwa wahudhuriaji wa tamasha hilo hawakupewa tahadhari yoyote kabla ya ajali hiyo iliyotokea katika jiji la Amritsar, jimbo la Punjab.
“Kulikuwa na kelele nyingi kwenye tamasha hilo, na inaonekana wahanga wa ajali hiyo hawakusikia mlio wa treni ilipokuwa inakaribia,” taarifa ya polisi kwa umma imeeleza.
“Hadi sasa watu zaidi ya 60 wamekufa. Lakini kipaumbele kilichopo hivi sasa ni kuhakikisha majeruhi wa ajali wanapatiwa matibabu husika hospitalini,” Kamisha wa Polisi wa jiji la Amritsar, S. S. Srivastava aliviambia vyombo vya habari.
Shuhuda wa ajali hiyo amesema kuwa walikuwa wanaangalia tamasha ambalo lilifana, ghafla waliona treni ikiwa kasi inasogelea umati na ndipo kila mtu alianza kukimbia.
Alisema wakati wanakimbia, treni ilivamia umati wa watu na kusababisha maafa huku mamia wakijeruhiwa.